Senata Miraj Ataka Kumbukumbu Kwa Waathiriwa Wa Mkasa Wa Feri,Likoni

Sunday, 29 March, 2026

Seneta Miraj Abdillahi amewasilisha Hoja katika Bunge la Seneti akitaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina kubaini idadi ya familia zilizoathirika kufuatia mkasa wa feri ya Likoni wa mwaka 1994.

Seneta Miraj anataka uchunguzi huo ufanywe ili kuhakikisha waathiriwa wote wanapata haki.

“Kamati ya Kudumu ya Seneti ya Barabara, Uchukuzi na Makazi ifanye uchunguzi wa kina ili kubaini idadi ya familia zilizoathirika, fidia iliyolipwa hadi sasa, madai yoyote ambayo hayajalipwa na kubainisha familia zipi bado hazijapata fidia na sababu za kutolipwa fidia hiyo,” alisema Seneta Miraj.

Alieleza kuwa licha ya hakikisho na ahadi zilizotolewa na mamlaka mbalimbali kufuatia janga hilo, bado kuna mashaka kuhusu iwapo fidia ilitolewa kikamilifu na kwa haki kwa familia zote zilizoathirika.

Aidha, Seneta huyo wa Chama cha UDA ameitaka Serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa kushirikiana na Wizara ya Barabara na Uchukuzi kuanzisha kumbukumbu ya kudumu kwa heshima ya wahanga wa ajali ya feri ya Likoni ya mwaka 1994.

“Kuanzishwa kwa kumbukumbu ya kitaifa ni hatua muhimu ya kuheshimu na kuwaenzi waliopoteza maisha na pia ni njia ya kuendeleza uponyaji wa pamoja wa kijamii na kuimarisha uwajibikaji wa Taifa kwa raia wake,” alikariri Seneta Miraj.

Kadhalika, Seneta huyo Maalum alielezea masikitiko kuhusu mkasa wa Aprili 29, 1994, akisisitiza umuhimu wa kuweka kumbukumbu ya kudumu kwa wahanga kama njia ya kuwaheshimu na kuwakumbuka.

“Janga la ajali ya feri ya Likoni lilisababisha vifo na majeraha kwa wananchi wasio na hatia, wengi wao wakiwa wakaazi wa Likoni na Kaunti ya Mombasa na hivyo kuleta majonzi makubwa kitaifa na madhara ya muda mrefu ya kimwili, kisaikolojia, kijamii na kiuchumi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na manusura,” alifafanua Seneta Miraj.

Hoja hiyo sasa itajadiliwa na Maseneta ili kutoa mwelekeo muafaka.