Usalama kuimarishwa kabla ya mazishi ya mwendazake Ong'ondo Were hapo kesho
Friday, 9 May, 2025
Kaunti ya HomabayAlhamisi Mei 8, 2025
Wito wa amani na utulivu umetolewa kabla ya mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Kasipul, Charles Ong’ondo Were, huku maandalizi ya mwisho yakiendelea katika Shule ya Sekondari ya Agoro Sare ambako watu walikusanyika kwa maombi, mahubiri, na kutazama mwili wa marehemu kwa mara ya mwisho.
Viongozi wa kisiasa wakiongozwa na Kamishna wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC), Mishi Mboko, walitoa wito wa kuimarishwa kwa usalama kutokana na hofu ya kuwepo kwa watu wanaopanga kuvuruga shughuli za mazishi kwa fujo.
Mbunge huyo ambaye aliheshimiwa kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya eneo la Kasipul, anatarajiwa kuzikwa kesho kwa heshima kubwa. Wakazi wa Kasipul wametakiwa kudumisha amani na kuenzi maisha ya Were kwa kutokubali kushiriki au kuunga mkono vurugu zozote.
“Hili ni tukio la heshima. Tujiepushe na chokochoko za kisiasa na tutumie fursa hii kumuenzi kiongozi wetu kwa amani,” alisema Mboko.
Mazishi hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa kitaifa na wa kaunti pamoja na wananchi kwa ujumla