Mswada wa Fedha wa 2025 (Finance Bill 2025)
Tuesday, 3 June, 2025
Utangulizi
Mswada wa Fedha (Mswada wa Bunge la Taifa Nambari 19 wa 2025) ni Mswada unaodhaminiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango ya Taifa, Mheshimiwa Kuria Kimani.
Mswada ulichapishwa tarehe 6 Mei 2025. Ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni na baada ya hapo, Kamati ya Fedha na Mipango ya Taifa ilikabidhiwa Mswada.
Ushirikishwaji wa Umma
Kamati inatakiwa kuuzingatia Mswada, kualika maoni kutoka kwa umma, na kuandaa ripoti yake na mapendekezo ya marekebisho yoyote inayoona yanafaa.
Katiba inatambua umuhimu wa kushirikisha umma katika kutoa maoni kuhusu masuala ambayo yanawaathiri. Hivyo, *Ibara ya 118(1) (b) ya Katiba ya Kenya* inaelekeza kwamba Bunge lazima iwezeshe ushirikishwaji wa umma na umma lazima ipewe fursa ya kutoa maoni kwenye Mswada kama huu.
Ushirikishwaji wa umma (public participation) ni agizo la kikatiba. Wananchi wako huru kutoa maoni yao kuhusu Mswada huu na wanaweza kuunga mkono Mswada au kupinga Mswada. La muhimu ni kutoa sababu ili Kamati ya Kiidara ya Fedha na Mipango ya Taifa ishughulikie kwa kina maoni yako.
Shughuli hii ya vikao vya umma vitaanza leo *Jumanne tarehe 3 Juni hadi Ijumaa tarehe 6 Juni, 2025* katika Kaunti zifuatazo: *Migori, Busia, Nandi, Trans Nzoia, Machakos, Kiambu, Mombasa, Kwale na Kilifi.*
Kuhusu Mswada wa Fedha
Mswada wa Fedha ni chombo cha kisheria cha kila mwaka kinacholenga kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali ya Taifa. Kulingana na Taarifa ya Sera ya Bajeti na Makadirio ya Bajeti yaliyoidhinishwa, Mswada huu unazingatia kuongeza mapato ya kodi kupitia marekebisho ya sheria za ushuru na uboreshaji wa utiifu wa walipa ushuru.
Kurahisisha sheria ya ushuru ni miongoni mwa mapendekezo muhimu ambapo kutakuwa na upunguzaji wa ugumu, na uondoaji wa vifungu visivyo vya lazima au vilivyopitwa na wakati, hivyo kuwezesha utiifu wa sheria.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 39A cha Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma, Sura ya 412A, Waziri wa Hazina ya Kitaifa ana wajibu wa kuwasilisha Mswada wa Fedha katika Bunge la Taifa. Mswada wa Fedha wa 2025 umetayarishwa kutokana na mazingira magumu ya kifedha, huku Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/26 ikiwa na fursa ndogo za ufadhili kutokana na kuongezeka kwa shinikizo la matumizi na nafasi ndogo ya hatua mpya za ushuru.
Ili kuziba pengo la kifedha, Mswada unakuja na mkakati unaolenga kuboresha ufanisi wa ukusanyaji mapato. Unahusisha marekebisho ya sheria na kurahisisha majukumu ya ushuru ili kuyafanya yaeleweke zaidi, hivyo kuhakikisha utiifu wa hali ya juu na kuondoa vifungu vya kisheria visivyo vya lazima.
Sambamba na *Mkakati wa Mapato wa Muda wa Kati (Medium Term Revenue Strategy)* na *Sera ya Kitaifa ya Ushuru (National Tax Policy)*, Mswada huu pia unalenga kurahisisha *vivutio vya kodi (tax incentives)* chini ya *Sheria ya Ada na Ushuru Mbalimbali ( Miscellaneous Fees and Levies Act), Sheria ya Ushuru wa Mapato (Income Tax Act),* na *Sheria ya Ushuru wa Ongezeko la Thamani (VAT Act)*.
Lengo ni kupunguza gharama za ushuru (tax expenditures) na kupanga mfumo wa ushuru kuelekea utendaji bora wa kimataifa.
Mswada unarekebisha sheria zifuatazo:
*1. Sheria ya Ushuru wa Mapato (Income Tax Act)*
*2. Sheria ya Ongezeko la Thamani ya Bidhaa (Value Added Tax Act)*
*3. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty Act)*
*4. Sheria ya Taratibu za Ushuru (Tax Procedures Act)*
*5. Sheria ya Ada Mbalimbali na Tozo( Miscellaneous Fees and Levies Act)*
*6. Sheria ya Ushuru wa Stempu (Stamp Duty Act)*